Watu waliokuwapo awamu zote za uongozi wa nchi wanaweza kuyaeleza vema zaidi mabadiliko yanayotokea katika sekta ya habari hapa nchini na duniani kwa ujumla.
Kwa ufupi, nguvu na umuhimu wa vyombo vya habari rasmi inazidi kupungua kila uchao kadri teknolojia ya mawasiliano inavyozidi kukua na kusambaa katika maeneo yote.
Zamani, enzi zile za Rais Julius Nyerere na baadaye Ali Hassan Mwinyi, vyombo vya habari vilikuwa ni kila kitu. Hakukuwa na njia nyingine rahisi ya kufikisha ujumbe kwa watu, kinyume na vyombo hivyo.
Wakati wa Nyerere, si ilikuwa si tu vyombo vya habari, bali ilikuwa vyombo vya Serikali, hususan magazeti na redio. Usipopewa nafasi enzi hizo, kelele zako zitaishia huko mtaani. Labda utengeneze vipeperushi na isingekuwa kirahisi kihivyo.
Wakati wa Mwinyi, tulianza kuona mabadiliko ya sera yaliyoruhusu vyombo binafsi, redio, magazeti. Vituo vya televisheni navyo vikaja. Nazungumzia Bara. Mabadiliko haya yaliwapa watu uwezo zaidi wa watu wenye fikra na mawazo mbadala kupata fursa ya kusikika kuliko zamani, lakini bado vyombo vya habari vilikuwa ni njia pekee ya kufikisha ujumbe kwa watu.
Ni katika kipindi cha awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa, mapinduzi ya vyombo vya kijamii huko duniani ndiyo yalianza kwa kufunguliwa tovuti iliyoitwa Six Degrees mwaka 1997, iliyowezesha watu kuweka wasifu wao na kukutana na marafiki.
Baada ya hapo, zikaanza blogu mwaka 1999. Hata hivyo, historia ya blogu Tanzania inaanzia mwaka 2004 pale mwanasheria na mwandishi wa habari Ndesanjo Macha alipoanzisha blogu ‘Jikomboe’ inayoaminika kuwa ndiyo ya kwanza ya Kiswahili.
Zilianzishwa blogu kadhaa kama Kisima cha Fikra na nyinezo. Sekta ya blogu ilipata nguvu kubwa na umaarufu mwaka 2005 (mwanzo wa utawala wa Kikwete) pale Issa Michuzi alipoanzisha blogu ya picha. Kwa maendeleo yaliyofikiwa sasa, blogu ni mtandao wa kijamii ambao ni ‘mhenga’. Hizi ni enzi za Instagram, Twitter, Facebook, Snapchat, Youtube nk.
Mabadiliko enzi za mtandao
Ukilinganisha na enzi zile, kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya habari. Kwa sasa, vyombo vya habari vya kijamii naweza kusema vinashindana na vyombo vikuu vya kizamani vya habari, redio, magazeti na televisheni. Huu ndiyo ukweli.
Siku hizi, haiwezekani kumnyima mtu nafasi ya kutoa ujumbe na mawazo yake kwa wanajamii, shukrani ziende kwa mitandao ya kijamii.
Hivi majuzi, Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa anahangaika kupambana na wabunge wanaotoa matamko mitandaoni wakimkosoa.
Zamani ingekuwa rahisi. Unawanyima tu nafasi ya kuongea kwa kutoa maagizo au vitisho kwa vyombo vya habari. Akinyimwa jukwaa la kuongelea, angeishia kupiga kelele mtaani kwake. Hakuna ambaye angemsikia.
Hayo hayawezekani dunia ya leo kwani mitandao ya kijamii inampa kila mtu nafasi ya kusema, apendavyo. Ukikataliwa na vyombo vikuu, huna haja hata ya kumuomba mtu. Unafungua akaunti na kubwabwaja utakavyo.
Ukuu wa kurasa maarufu
Ukweli mpya ni kuwa watu maarufu wana ufuasi mkubwa, wanasomwa kuliko vyombo vingi vya habari.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwa ujumla, vyombo vya habari yaani redio, televisheni na magazeti vimepoteza mapato ya matangazo kwa mitandao ya kijamii. Inawezekana kuna baadhi ya nchi, au vyombo fulani katika nchi husika, ambavyo vinafanya vizuri, lakini ukweli wa jumla ndio huo.
Mtangazaji akitaka kutangaza bidhaa yake iwafikie watu ataenda katika kurasa za watu maarufu, zenye wafuasi kwa mamilioni, hususan wasanii ambao kupitia wao unaweza kufikia watu wengi kuliko magazeti au redio nyingi ambayo labda husomwa au husikilizwa na mamia au maelfu.
Faida pekee ambayo vyombo vikuu inayo ni hadhi na heshima.
Kwamba mitandao ya jamii kwa ujumla wake inaonekana imejaa uongo, uhuni, matusi, kurasa feki, watu wasiojulikana nk. Faida nyingine kwa redio pekee ni kuwa ni bure kusikiliza, huhitaji MB na inafikia hata wasiojua kusoma na watu wa vijijini.
Mitandao ya kijamii imekuwa ikizalisha habari kubwa zinazotawala kurasa za mbele za magazeti, mara nyingi.
Wanasiasa wakubwa na machachari, siku hata hawana haja ya kuitisha mikutano ya habari. Wanaandika mawazo yao katika kurasa zao, na waandishi huchukua. Haya ni mapinduzi makubwa.
Mitandao ya kijamii imekuwa muhimu sana kiasi kwamba unaweza usiangalie habari siku nzima, lakini usipitwe na kitu iwapo upo kwenye mitandao.
Siku hizi hata habari za vituo vingi hurushwa mbashara katika mitandao ya kijamii.
Binafsi nikiwa ofisini, kama kuna tukio kubwa linaendelea na linarushwa moja kwa moja, basi nitaliangalia kupitia mitandao ya kijamii. Nakumbuka hata taarifa zote mbili za makinikia niliziangalia kupitia YouTube.
Mitandao ya kijamii inatupatia fursa kubwa ya kufikia maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kiuchumi, mitandao imeajiri watu wengi. Hivi sasa, shukrani kwa teknolojia hii, mamia ya watu wanapata mkate wao wa kila siku. Tusingekuwa tunazungumzia kampuni ya habari ya Millard Ayo na nyingine nyingi, bila mitandao, achilia mbali mamilioni ya pesa yanayoingia kwa watu kupitia matangazo.
Mitandao ya kijamii imerahisisha maisha ya watu. Kwa sasa, ni rahisi kupata taarifa za upatikanaji wa huduma mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii. Haja ya kusafiri ili kufanya biashara imepungua kwa hiyo mitandao pia imeokoa muda wa kusafiri.
Ubaya wa mitandao
Hivi majuzi nilikuwa katika ofisi ya ardhi pale Magomeni nikakutana na mzee mmoja wa zaidi ya miaka 60 wakati tukisubiri huduma. Katika mazungumzo, mzee alianza kutupia lawama mitandao ya kijamii kuwa haina faida yoyote zaidi ya kuharibu maadili na kuchafua jamii.
Wakati mzee anazungumza hayo, nilikuwa katika kundi la WhatsApp nikiendelea na majadiliano na waandishi wenzangu wa gazeti moja la wiki ninalolifanyia kazi muda wa ziada. Bila teknolojia hii, tungelazimika kukutana ana kwa ana kujadili mambo yetu. Ingekuwa ni kupoteza muda. Nikawaza mzee huyu ni katika watu waliokataa kubadilika kutokana na wakati. Amekwama katika zama za Nyerere. Ni bahati mbaya sana.
Hata hivyo, malalamiko ya mzee wangu yule si ya kupuuza moja kwa moja hata kidogo, ingawa suluhu si kuikataa teknolojia hii iliyoleta mapinduzi makubwa, bali kudhibiti matumizi yake, hususan katika ngazi ya mtu binafsi na kazini. Katika malalamiko yake, mzee alisema watu wanachati maofisini badala ya kufanya kazi, jambo ambalo ni la kweli kabisa. Pia, mzee alilalamika kuwa watu hutumia mitandao kuangalia na kutumiana picha za matusi. Pia, ni kweli. Zaidi ya hapo, alisema watu wamekuwa kama machizi, ambapo si ajabu kukuta wanacheka cheka hivyo, huku wakibofya bofya simu zao. Hii nayo ni kweli, ingawa sina hakika kama ni jambo baya.
Mitandao ina faida nyingi nilizozitaja tayari, lakini pia ina athari zake kubwa. Natamani tungeweza kudhibiti athari hizo ili mitandao isiwe sababu ya kurudisha nyuma maendeleo yetu. Kama alivyosema mzee, maeneo ya kazi, mfanyakazi yafaa asiruhusiwe kabisa kuingia na simu, lakini hii pia inategemea aina ya kazi.
Nchi nyingine na baadhi ya maofisi hapahapa Dar es Salaam, hususan katika balozi na taasisi za kimataifa, zinafanya hivyo. Watu wasiruhusiwe kuingia maofisini na simu, isipokuwa wale ambao kazi zao zinahitaji matumizi ya simu. Na hata hao, zitumike za ofisi.
Watanzania tunapenda umbeya na kufuatilia maisha ya watu wetu maarufu. Hivi majuzi mwanamuziki Diamond alipojitokeza katika redio kukiri kuwa amechepuka, mitandao ya kijamii ilichangamka. Watu walishinda huko kuangalia Zari kajibu nini, Hamisa anasemaje, Mange naye ametoa maoni gani na kufuatilia mijadala mbalimbali. Achilia mbali waliotoa maoni, kuna maelfu wanaosoma tu mijadala. Kazi zilifanyika sawasawa kweli?
Hawa wanaokesha mitandaoni ndiyo watumishi wetu wa umma na katika maofisi binafsi. Hawa ndiyo wenye uwezo wa kununua au kupata bure MB na hawa ndiyo wenye maarifa ya kutumia mitandao. Ni muda muafaka sasa, tudhibiti hili.
Mitandao ya kijamii ni jukwaa la mijadala, lakini mijadala yenyewe inayoongoza ikiwa ni kuhusu maisha ya watu, sina hakika kama tutafaidika sana.
Mitandao ya kijamii inapoteza muda wetu mwingi kwa sababu ina uraibu wa ajabu. Ukifungua ukurasa huu mara umehamia hapa, ukishtuka saa nzima imekwenda ukisoma posti za Wolper na Harmonize, Jux na Vanessa, Hamisa na Zaari wakirushiana madongo.

No comments:
Post a Comment