Shindano la Top 100 lazinduliwa Mbeya - HD NEWS

Breaking

Habari za Uhakika

Socialize

Wednesday

Shindano la Top 100 lazinduliwa Mbeya


Shidano la kusaka kampuni bora 100 za kiwango cha kati (Top 100) kati kwa mwaka huu limewafikia wafanyabiashara wa mkoani Mbeya baada ya kuzinduliwa rasmi jana huku likielezwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwa kampuni nyingi nchini.
Uzinduzi wa shindano hilo ambalo linadhaminiwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), kupitia gazeti lake la The Citizen na kampuni ya KPMG mkoani Mbeya uliwashirikisha wafanyabiashara kutoka kampuni zaidi ya 25.
Akizungumza katika uzinduzi huo, mwakilishi wa kampuni ya KPMG, Ketan Shah alisema  kampuni hizo zimeamua kuwafuata wafanyabiashara wa kampuni za kati mkoani Mbeya  kuwahamasisha ili washindanishe kampuni zao ikiwa ni njia moja ya kutambulika ndani na nje ya nchi.
Alitaja vigezo vinavyotumika kupata washindi kuwa ni mapato ya kampuni husika, idadi ya wafanyakazi walioajiriwa, ulipaji wa kodi serikalini na uwezo wa kupanua biashara mpaka nje ya nchi.
“Tunawakaribisha wafanyabiashara wenye kampuni za kati kushiriki shindano hili kwani hii itasaidia kwenu pia kujitangaza na kutambulika, lakini pia kutambua mwenendo wa uchumi wa Taifa,” alisema.
Mwakilishi wa MCL, Ndika Maliatabu alizipongeza kampuni  zilizojitokeza katika  uzinduzi huo ulioambatana na elimu kwa mlipakodi na jinsi ya kujiunga katika shidano hilo akisema ni hatua moja ya kujipima uwezo kwa kujilinganisha na nyingine.
Alisema kupitia shidano hilo, wafanyabiashara watakutana pamoja na kubadilishana mawazo. Pia, alisema hiyo ni fursa ya kutambua wajibu na haki zao katika biashara kwa kupata elimu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Na sisi Mwananchi Communications tunawakaribisha kuja kutangaza bidhaa au kampuni zenu kwenye magazeti yetu ambayo yanasomwa na watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi,” alisema.
Ofisa Mkuu wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Julius Mjenga aliwatoa hofu wafanyabiashara hao kwamba kujiunga kwao katika shindano hilo kutawafanya wabanwe na TRA kuhusu mapato huku akibainisha kuwa suala la kulipa kodi lipo kwa mujibu wa sheria na kila mfanyabiashara atalipa kwa taratibu zilizopo.
Aliwahimiza wafanyabiashara hao kuchangamkia shindano hilo la kusaka kampuni  100 bora za kati huku wakitunza kumbukumbu za mauzo yao ili kuepuka msuguano au kukadiriwa mapato tofauti.
Mwakilishi wa kampuni ya  Ajim Enterprises Ltd, Peter Mwampondele alisema elimu waliyopata kutoka kwa waandaaji wa shindano hilo inaonyesha dira ya fursa kubwa katika kampuni zao kwani itawafanya watambulike sehemu kubwa katika jamii.
“Hii ni fursa ya pekee kwetu wafanyabiashara, kwanza kujitangaza sisi wenyewe kama ambavyo tumewasikia kwamba tukitumia vyombo vya habari kama vile magazeti ya Mwananchi itatufanya tusonge mbele zaidi kibiashara,” alisema Mwampondele.

No comments:

Post a Comment